Kisukari cha ujauzito kinasababishwa na nini?
Medikea
Kisukari cha ujauzito kinasababishwaje?
Kisukari cha ujauzito ni ugonjwa wa kisukari unaogunduliwa kwa mara ya kwanza wakati wa ujauzito. Hutokea wakati mwili unaposhindwa kutoa insulini ya kutosha (homoni inayosaidia kudhibiti viwango vya sukari kwenye damu) ili kukidhi mahitaji ya ziada wakati wa ujauzito.
Kisukari cha ujauzito huweza kutokea katika kipindi chochote cha ujauzito, lakini kwa kawaida hutokea katika miezi 6 au miezi 9 ya ujauzito. Baada ya mama mjamzito kujifungua sukari yake ya damu hurudi katika kiwango chake cha kawaida. Lakini ikiwa amewahi kuwa na kisukari cha ujauzito kabla ana hatari kubwa ya kupata kisukari cha aina ya pili hivyo, atahitajika kupima mabadiliko katika sukari ya damu mara nyingi zaidi.
Je, nani yupo kwenye hatari zaidi ya kupata kisukari cha ujauzito?
Mwanamke yeyote anaweza kupata kisukari cha ujauzito wakati wa ujauzito, lakini mwanamke mjamzito aliyeko kwenye hatari zaidi ni mwenye mambo yafuatayo;
- Historia ya ugonjwa wa kisukari katika familia
- Uzito au unene kupita kiasi
- Historia ya kisukari cha ujauzito katika ujauzito uliopita
- Umri zaidi ya miaka 40
- Baada ya kujifungua mtoto mwenye uzito wa zaidi ya kilo 4.1
Dalili za ugonjwa wa kisukari cha ujauzito;
Mara nyingi ugonjwa wa kisukari cha ujauzito huwa hauonyeshi dalili za wazi hivyo wengi uugundua pale wanapoenda kufanya uchunguzi wa viwango vya sukari kwenye damu wakati wa ujauzito. Japo ikiwa viwango vya sukari kwenye damu vitabaki juu kwa muda mrefu mwanamke huweza kuona dalili zifuatazo;
- Kukojoa mara nyingi zaidi kuliko kawaida
- Uchovu
- Kiu kupita kiasi
- Njaa iliyokithiri
- Kutoona vizuri
- Kinywa kikavu
- Maambukizi ya mara kwa mara kwenye uke
Baadhi ya dalili hizi huweza kuwa za kawaida wakati wa ujauzito na si lazima kuwa ishara ya ugonjwa wa kisukari cha mimba hivyo ni vyema kuwasiliana na mtoa huduma ya afya(mkunga) kuhusu dalili hizo na kufanya uchunguzi ili kupata majibu sahihi zaidi.
Je, madhara ya kisukari cha ujauzito ni yapi?
Ugonjwa wa kisukari cha ujauzito usipodhibitiwa mapema huweza kusababisha viwango vya juu vya sukari ya damu ambavyo huweza kusababisha shida kwa mama na mtoto kama ifuatavyo;
- Mtoto kukua zaidi kuliko kawaida
- Kuzaa kabla ya wakati
- Matatizo ya kupumua kwa mtoto
- Mtoto kupata sukari ya chini ya damu au kuwa na ngozi na macho ya njano baada ya kuzaliwa
- Kifo cha mtoto kabla au muda mfupi baada ya kuzaliwa
- Shinikizo la damu kwa mama mjamzito
- Kujifungua kwa upasuaji
- Ugonjwa wa kisukari wa baadae
Matibabu ya ugonjwa wa kisukari cha ujauzito.
- Ufuatiliaji wa viwango vya sukari kwenye damu
- Kula vyakula vyenye afya
- Kufanya mazoezi ya mwili
- Kufuatili ukuaji wa mimba yako
- Matumizi ya dawa kulingana na maelekezo ya mtoa huduma ya afya. Kwa mfano vidonge vya kumeza na sindano za insulini
Nini cha kuzingatia baada ya kujifunga
Pamoja na tatizo la kisukari cha ujauzito kuisha baada ya kujifungua ni vyema mwanamke kubadili mtindo wake wa maisha kwa kula vyakula vyenye afya na kufanya mazoezi, pia kuendelea kufuatilia kiwango chake cha sukari kwenye damu.