Genital Warts (Masundosundo): Tiba na jinsi ya kujikinga

Medikea

Medikea

Genital Warts (Masundosundo): Tiba na jinsi ya kujikinga

Masundosundo (Genital warts) ni ugonjwa gani?

Ugonjwa wa genital warts ni hali ya kuota vinyama maeneo ya sehemu za siri kama vile kwenye uume, kuta za uke, mirija ya mkojo (urethra), shingo ya kizazi (cervix), au maeneo ya kuzunguka njia ya haja kubwa au ndani ya njia ya haja kubwa. Pia vinyama hivi vinaweza kuota mdomoni au kwenye koo la mtu ambaye amefanya ngono ya mdomo na mtu mwenye maambukizi.

Je, genital warts au masundosundo husababishwa na nini?

Tatizo la kuota vinyama sehemu za siri au masundosundo husababishwa na virusi aina ya human papillomavirus (HPV),ambavyo kwa asilimia kubwa huenezwa kwa njia ya kujamiiana, lakini pia mtu huweza kupata virusi hivyo kwa kugusana kimwili hasa maeneo ya utupu na mtu aliyenavyo. Virusi vya HPV vinavyoweza kusababisha maambukizi kwenye via vya uzazi vya wanaume na wanawake vipo vya aina zaidi ya 40. Aina ya virusi vinavyosababisha masundosundo (genital warts) ni HPV 6 na HPV 11.

Je, nani yupo kwenye hatari zaidi ya kupata ugonjwa wa masundosundo?

Makundi yaliyopo kwenye hatari zaidi ya kupata masundosundo  ni pamoja na; 

  • Watu wenye wapenzi wengi. 
  • Wanaofanya ngono isiyosalama.
  • Wanaoanza kujamiiana katika umri mdogo. 
  • Wenye upungufu katika mfumo wa kinga mwilini kwa sababu ya magonjwa mbalimbali kama vile UKIMWI.

Dalili za ugonjwa wa masundosundo ni zipi?

Dalili za ugonjwa masundosungo ni pamoja na; 

  • Kuota vinyama sehemu za siri kwenye uume au uke, na sehemu za nje na ndani ya haja kubwa.
  • Kutokwa na uchafu na kuwashwa sehemu za siri. 
  • Kutokwa na damu wakati wa tendo la ndoa au baada ya tendo la ndoa.

Hata hivyo watu wengi huwa hawaoneshi dalili zozote za ugonjwa ingawa wanaweza kuwaambukiza wenzi wao bila wao kujua, hivyo uchunguzi na vipimo vya hospitali ni muhimu ili kufahamu kama kuna masundosundo na kupata matibabu ya haraka.

Jinsi ya kutibu tatizo la genital warts au  masundosundo?

Tatizo la vinyama vya sehemu za siri linaweza kutibiwa na kuondolewa japo wakati mwingine hutokea tena. Matibabu ya  masundosundo ya sehemu za siri ni pamoja na;

Dawa ya kupaka kwa juu moja kwa moja kwenye vinyama (warts) kulingana na maelekezo ya daktari. (cream, liquid or ointment)

Kutumia nitrojeni ya maji ambayo huwekwa na daktari kuzunguka vinyama (warts) ambavyo hatimaye huanguka (cryotherapy)

Kuondoa warts kwa kutumia umeme. (Electrocautery)

Kuondoa warts kwa njia ya upasuaji. (surgery)

Hitimisho

Kuchelewa kupata matibabu ya masundosundo (genital warts) kunaweza kusababisha madhara mbalimbali kwa mgonjwa kama vile; saratani katika maeneo ya maambukizi, ugumu wakati wa kujifungua, usambazaji wa maambukizi kwa mtoto wakati wa kujifungua na vidonda katika sehemu za uzazi.

Unaweza kuchat na daktari moja kwa moja ukiwa nyumbani kwako ili kupata ushauri na tiba stahiki kupitia Medikea App